Na Neema Joseph
Mwanza
Baadhi ya watoto yatima jijini Mwanza wameangukia katika janga la unyanyasaji wa kijinsia bila jamii kujua vitendo vinavyoendelea katika maeneo ya watoto hao wa mitaani hali maarufu kama (Ghetto).
Ilikuwa ni usiku wa saa tano hivi nilifanikiwa kujichanganya na kundi moja la watoto hao wa mitaani, huku nami nikijifanya ni muumini wa makundi hayo, nakumbuka ilikuwa ni wa mtaa mmoja katika barabra ya Nyerere, kando ya barabara hizo utakutana na nyumba za ghorofa, maeneo hayo ndiyo makazi ya watoto hao wa mitaani pamoja na maeneo mengine jijini Mwanza.
Wakati nilipokuwa katika kundi hilo la watoto wa kike walishuhudia mwenzetu mmoja akifanyiwa unyama mkubwa, kwani lilitokea kundi jingine la wavulana watatu na kisha kusogelea kundi hilo na kuamua kumchukua binti mmoja ambaye alikuwa amekaa karibu na barabara na kisha kuingia naye kwenye uchochoro na baada ya muda ilisikika sauti ya binti yule ikiomba msaada.
Licha ya kelele zile zilizoashiria kufanyiwa vitendo viovu vya kubakwa, baadhi ya watu waliokuwa kipita eneo lile waliendelea na shughuli zao bila hata kuona huruma kwa kwenda kutoa msaada. Nafikiri hali hiyo inatokana na historia ya vikundi hivyo kuwa ni vya kinyama na vinatembea na silaha mbalimbali vikiwemo visu , nyembe na hata panga.
Bila shaka unyama huo aliotendewa binti huyo kwa mujibu wa Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA), ukatili huo unaangukia katika kundi la ukatili wa saikolojia na unaweza kusababisha mhusika kujinyonga.
Hapo ndipo nilipomuuliza mmoja wa marafiki wale niliokuwa nao sehemu ile naye akiwa ni mtoto wa mitaani, aliniambia kuwa hali hiyo ni ya kawaida katika maisha yake ya mitaani na wao wameyazoea . Hapo ndipo nilipotaka kujua msaada wowote wanaoupata hasa kutoka kwa askari wa doria, ndipo binti huyo aliyejitambulisha kwa jina Mary , ikiwa ni jina la bandia nililompa aliniambia kuwa hakuna msaada wowote wanaoupata kwa askari wanaokuwa doria, pindi wanapofanyiwa vitendo hivyo katili
Hapo nilizidi kupata picha nyingine tofauti kwa kujiuliza inakuwaje hata mamlaka za usalama kama jeshi la polisi kutotambua unyama huo wa watoto wa mitaani ?. Kimsingi kunakuwa na makundi mengi ya watoto hao wa mitaani, wanazidiana kwa rika na umri, hivyo wale wakubwa wanakuwa na sauti dhidi ya wale wadogo wanaoingia kwenye maisha hayo.
Pia uchunguzi wangu ulibaini kuwepo kwa vyeo ndani ya makundi hayo, kuna wanaojiita King, ikiwa ndiyo viongozi wa makundi, na kuna wale wa ngazi ya kati wanaotumwa na viongozi wao hasa kwenda kufanya uhalifu sehemu fulani na kuleta watakachokipata huko.
Katika ukatili wa jinsia makundi hayo yanahusika kwa kiasi kikubwa, kwani king au mtawala anapohitaji kufanya tendo la ngono, basi atatoa amri ya kuletewa binti katika maskani yake na wale wa kati watatekeleza jukumu hilo kwa kuhofia kupatwa na adhabu kama watashindwa kutekeleza jukumu hilo.
Ni muda muafaka sasa jamii kusimama na kuungana na Chama cha Waandishi wa Habari wanawake Tanzania (TAMWA )kupinga ukatili huo wanaofanyiana watoto hao wa mitaani .
Nazo takwimu za benki ya dunia zinaonyesha kuwa wanawake wenye umri wa kuanzia miaka 15 – 44 wapo katika hatari kubwa ya kubakwa kuliko kuugua saratani, kupata ajali , vita na mlaria.
Pia licha ya sheria ya nchi inayoeleza kuwa endapo mtu atabainika kuhusika kufanya ubakaji atahukumiwa miaka thelathini jela, lakini bado vitendo hivyo vinaendelea, lakini swali la msingi ni nani anasimamia vitendo hivyo kwa makundi kama watoto wa mitaani? Je watoto hao wa mitaani wamepewa elimu ya kuripoti vitendo hivyo vya kinyama.